Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Maulana Sheikh Hemed Jalala aliyasema hayo katika khutuba yake ya Ijumaa, iliyoswaliwa jana tareh 23 Oktoba 20216 sawa na tareh 1 Aban 1405 H.S, ambapo alielezea umuhimu wa kuwaheshimu wazazi, kumchagua mwenza mwema wa maisha na kuzingatia malezi ya watoto tangia hatua za awali za kuanzisha familia.
Sheikh Jalala alianza khutuba yake kwa kusoma aya ya Qur’ani Tukufu inayozungumzia wajibu wa kuwaheshimu wazazi na kuwaombea rehema, akisema:
﴿ وَٱخۡفِضۡ لَهُمَا جَنَاحَ ٱلذُّلِّ مِنَ ٱلرَّحۡمَةِ وَقُل رَّبِّ ٱرۡحَمۡهُمَا كَمَا رَبَّيَانِي صَغِيرًا ﴾
“Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma, na useme: Mola wangu Mlezi! Warehemu kama walivyonilea nilipokuwa mdogo.”
(Suratul Isrāʾ, aya ya 24).
Akifafanua aya hiyo, Sheikh Jalala alisema kuwa: Mtoto ana wajibu wa kuwanyenyekea wazazi wake wawili na kuwatendea wema, pamoja na kuwaombea rehema kwa Mwenyezi Mungu, kama inavyoelekezwa katika sehemu ya aya inayosema:
وَقُل رَّبِّ ٱرْحَمْهُمَا كَمَا رَبَّيَانِي صَغِيرًا.
Alisisitiza kuwa mwanadamu anapaswa kutambua mchango mkubwa wa wazazi wake katika maisha yake, kwani walimlea, wakamtunza na kufanya juhudi mbalimbali kwa ajili ya ustawi wake tangia alipokuwa mdogo.
Mkurugenzi wa Hawza ya Imam Swadiq (as) aliongeza kuwa: Wajibu wa mtoto kwa wazazi wake hauishii wanapokuwa hai pekee, bali unaendelea hata baada ya kufariki kwao. Hivyo, watoto wanapaswa kuendeleza wema kwa wazazi wao kwa kuwaombea dua na kuwaombea rehema za Mwenyezi Mungu hata pindi wanakuwa wamefariki.
Malezi Bora Huanza Kabla ya Ndoa
Katika sehemu nyingine ya khutuba yake, Sheikh Jalala alieleza kuwa; safari ya kumlea mtoto mwema huanza kabla hata ya mtoto huyo kuzaliwa, akibainisha kuwa uchaguzi wa mwenza wa maisha ni hatua muhimu inayopaswa kuzingatiwa kwa makini.
Aliongeza kwa kusema: Mtu anayetaka kuanzisha familia anapaswa kuzingatia maadili na mwenendo wa familia anayotaka kuingia, kwa kuwa mazingira ya kifamilia yana nafasi muhimu katika malezi na makuzi ya watoto.
Aidha, aliwashauri vijana wanaotarajia kufunga ndoa kuwashirikisha wazazi wao katika maamuzi hayo muhimu, huku akiwahimiza kumuomba Mwenyezi Mungu awaongoze katika kuwapata wenza wema wa maisha yao.
Sheikh Jalala pia alisisitiza umuhimu wa kuchagua mwenza mwenye uchamungu, huku akieleza kuwa dini na maadili mema ni miongoni mwa mambo yanayopaswa kupewa uzito mkubwa katika uamuzi wa kuoa, kwa kuwa msingi wa familia una mchango muhimu katika malezi ya kizazi kijacho.
Malezi ni Hatua Muhimu katika Kumjenga Mtoto Mwema
Akiendelea kufafanua mada hiyo, Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania alisema kuwa: Baada ya hatua ya kumchagua mwenza mwema wa maisha, malezi yanakuwa sehemu muhimu katika safari ya kumjenga mtoto mwenye tabia njema na maadili yanayokubalika.
Alibainisha kuwa; kipindi cha malezi ni hatua nyeti sana katika maisha ya mtoto, hivyo wazazi wanapaswa kutimiza wajibu wao kwa umakini, kwa kumpa mtoto mwongozo unaofaa na kumkuza katika mazingira yanayomsaidia kujenga tabia njema.
Alisisitiza kuwa malezi ya watoto yanahitaji uangalizi na juhudi za makusudi kutoka kwa wazazi, kwani kujenga kizazi chenye maadili mema kunahitaji kuanza mapema na kuendelea katika hatua mbalimbali za ukuaji wa mtoto.
Katika kuhitimisha khutuba yake, Maulana Sheikh Hemed Jalala Mwakindenge, alimuomba Mwenyezi Mungu aijaalie jamii kheri, awaongoze wazazi katika kutimiza wajibu wao wa malezi na awajaalie watoto wawe wema, wenye kuwaheshimu wazazi wao na kushikamana na maadili mema.
Maoni yako